Hukumu Ya Mungu
1
Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana
katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe
kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo. 2 Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli. 3Hivyo wewe mwanadamu, utoapo hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu? 4 Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba?
5
Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu,
mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu
ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. 6 Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. 7
Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima
na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. 8
Lakini kwa wale watafutao mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na
kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. 9 Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, 10 bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. 11 Kwa maana Mungu hana upendeleo.
12
Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria,
nao wote wale waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria.
13
Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za
Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki. 14
(Naam, wakati wa watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanapofanya kwa
asili mambo yatakiwayo na sheria, wao ni sheria kwa nafsi zao wenyewe,
hata ingawa hawana sheria. 15
Wao wanaonyesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye
mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye
kupingana yatawashtaki au kuwatetea.) 16 Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo, kama isemavyo Injili yangu.
Wayahudi Na Sheria
17 Tazama, wewe ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea sheria na kujisifia uhusiano wako na Mungu, 18 kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo sheria, 19 kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani, 20 mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo sheria, 21 basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba? 22 Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu? 23Wewe ujivuniaye sheria, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja sheria? 24 Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu wa Mataifa.”
25 Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii sheria, lakini kama unavunja sheria, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. 26
Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo sheria inataka,
je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa? 27
Ndipo wale ambao hawakutahiriwa kimwili lakini wanaitii sheria
watawahukumu ninyi, ambao ingawa mmetahiriwa na kuijua sana sheria ya
Mungu iliyoandikwa, lakini mwaivunja.
28 Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili. 29
Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani, nayo tohara ya kweli ni jambo la
moyoni, ni la Roho, wala si la sheria iliyoandikwa. Mtu wa namna hiyo
hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.
JIBU MASWALI.