Kutii Mamlaka
 1 Kila mtu na atii mamlaka inayotawala, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, nazo mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. 2
                                Kwa hiyo yeye anayeasi dhidi ya mamlaka inayotawala anaasi dhidi ya
                                kile kilichowekwa na Mungu, nao wale wafanyao hivyo watajiletea hukumu
                                juu yao wenyewe. 3
                                Kwa kuwa watawala hawawatishi watu wale wanaotenda mema bali wale
                                wanaotenda mabaya. Je, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Basi tenda lile
                                lililo jema naye atakusifu. 4
                                Kwa maana mwenye mamlaka ni mtumishi wa Mungu kwa ajili ya mema. Lakini
                                kama ukitenda mabaya, basi ogopa, kwa kuwa hauinui upanga bila sababu.
                                Yeye ni mtumishi wa Mungu, mjumbe wa Mungu wa kutekeleza adhabu juu ya
                                watenda mabaya. 5 Kwa hiyo ni lazima kutii wenye mamlaka, si kwa sababu ya kuogopa adhabu iwezayo kutolewa, bali pia kwa ajili ya dhamiri.
 6 Kwa sababu hii mnalipa kodi, kwa maana watawala ni watumishi wa Mungu, ambao hutumia muda wao wote kutawala. 7
                                Mlipeni kila mtu kile mnachodaiwa. Kama mnadaiwa kodi lipeni kodi, kama
                                ni ushuru, lipeni ushuru, astahiliye hofu, mhofu, astahiliye heshima,
                                mheshimu.
Kupendana Kila Mmoja Na Mwingine
 8 Msidaiwe kitu na mtu yeyote, isipokuwa kupendana, kwa maana yeye ampendaye mwenzake, ameitimiza sheria. 9
                                Kwa kuwa amri hizi zisemazo, “Usizini,” “Usiue,” “Usiibe,” “Usitamani,”
                                na amri nyingine zote, zinajumlishwa katika amri hii moja: “Mpende
                                jirani yako kama nafsi yako.” 10 Upendo haumfanyii jirani jambo baya. Kwa hiyo upendo ndio utimilifu wa sheria.
 11
                                Nanyi fanyeni hivi, mkiutambua wakati tulio nao. Saa ya kuamka kutoka
                                usingizini imewadia, kwa maana sasa wokovu wetu umekaribia zaidi kuliko
                                hapo kwanza tulipoamini. 12 Usiku umeendelea sana, mapambazuko yamekaribia. Kwa hiyo tuyaweke kando matendo ya giza na tuvae silaha za nuru. 13
                                Basi na tuenende kwa adabu kama inavyopasa wakati wa mchana, si kwa
                                kufanya karamu za ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa
                                ugomvi na wivu. 14 Bali jivikeni Bwana Yesu Kristo, wala msifikiri jinsi mtakavyotimiza tamaa za miili yenu yenye asili ya dhambi.
JIBU MASWALI.
										
																					
			